Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha tarjuma cha Shirika la Habari la Hawza, vikosi mamluki na wanamgambo wa kiraia wanaohusishwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Bahrain, kwa kuweka mzingiro na vikwazo vikali vya kiusalama katika mji wa Al-Diraz ulioko magharibi mwa Manama, mji mkuu wa Bahrain, vilizuia Mashia kuadhimisha Swala ya Ijumaa ya pamoja kwa wiki ya themanini na nane mfululizo.
Vikosi hivyo mamluki, vikisaidiwa na magari ya kijeshi na wanajeshi wenye silaha na vifaa kamili, viliongeza uwepo wao katika maeneo yanayozunguka Msikiti wa Imam Sadiq (as), hatua hiyo ilichukuliwa kwa lengo la kukabiliana na uwezekano wa kuanza maandamano ya wananchi ya kupinga mzingiro wa kiusalama na kidini uliowekwa dhidi ya alama za madhehebu ya Kishia, kuonesha mshikamano na wafungwa wa kisiasa, pamoja na kupinga kuhalalishwa mahusiano na utawala wa Kizayuni na uwepo wa kijeshi wa Marekani nchini humo.
Katika maeneo mengi ya Bahrain pia, licha ya mzingiro mkali wa kiusalama, maandamano ya wananchi yalifanyika, waandamanaji katika mikusanyiko hiyo walitaka “magereza yawe matupu” na kuachiwa huru mara moja wanazuoni wote wa Kishia na wafungwa wa kisiasa. Aidha walilaani hatua ya utawala wa Bahrain ya kuzuia Mashia kuswali Swala ya Ijumaa, kuingilia rasmi masuala ya dini, na kuendelea kuweka vikwazo dhidi ya uhuru wa kidini katika kipindi kinachokaribia msimu wa Ashura (mwezi wa Muharram).
Waandamanaji walitaka kukomeshwa kwa sera za unyanyasaji wa kimadhehebu na ubaguzi dhidi ya Mashia, pamoja na kusitishwa mashambulizi dhidi ya viongozi, shakhsia, taasisi na misingi yote ya Madhehebu ya Jaafaria.
Pia walisisitiza msimamo wao wa kuiunga mkono Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika vita vyake vya kuzuia na kukabiliana na uchokozi wa Marekani na Uzayuni, na wakatangaza uaminifu wao kwa “Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Imam Sayyid Ali Khamenei” na Katibu Mkuu Shahidi wa Hizbullah ya Lebanon, “Sayyid Hassan Nasrallah”. Vilevile walitaka kukomeshwa uwepo wa Marekani nchini humo na kuondoshwa kambi za kijeshi za kigeni ili kuwezesha kupatikana kwa mamlaka kamili ya kitaifa na usalama wa ndani wa nchi.
Kadhalika walisisitiza ulazima wa kufutwa kwa makubaliano ya kuhalalisha mahusiano na adui Mzayuni, kufukuzwa kwa balozi wa utawala huo kutoka nchini, na kufungwa ubalozi wake mjini Manama.
Mamlaka za Bahrain zimekuwa zikipiga marufuku kufanyika kwa Swala ya Ijumaa tangu tarehe 4 Oktoba 2024 (1403 Shamsia). Hatua hiyo ilifuatia msisitizo wa wananchi wa kuandaa hafla za kumuenzi Sayyid Hassan Nasrallah, Katibu Mkuu Shahidi wa Hizbullah ya Lebanon, kufanya maandamano ya kuunga mkono nyanja za Muqawama wa Kiislamu nchini Lebanon, Palestina na Yemen, pamoja na kupinga makubaliano ya kuhalalisha mahusiano na utawala wa Kizayuni.
Maoni yako